Watu kadhaa wameripotiwa kujeruhiwa vibaya huku mali ya thamani ikiharibiwa baada ya wafuasi wa rapa Toxic Lyrikali na kundi la Buruklyn Boyz kukabiliana vikali katika eneo la Donholm, jijini Nairobi.
Mashuhuda wanasema purukushani hizo zilianza kwa mabishano makali yaliyogeuka kuwa vurugu, huku baadhi ya vijana wakirushiana mawe na kuharibu mali. Polisi walilazimika kufika haraka eneo la tukio ili kutuliza hali na kuzuia vurugu hizo kuenea zaidi.
Vurugu hizo zinadaiwa kuchochewa na bifu kali linaloendelea kati ya Toxic Lyrikali na Buruklyn Boyz. Mgogoro wao ulianza baada ya Toxic kuwatuhumu Buruklyn Boyz kukosa ubunifu na kuiga mtindo wake wa Trap Dancehall, madai ambayo yalipingwa vikali na kundi hilo.
Katika kuonyesha uwezo wao wa kimuziki, kila upande umeachia diss track kali zikilenga kushushiana hadhi na kuthibitisha nani ana ushawishi mkubwa kwenye soko la muziki wa mtaa.