Msanii nyota wa muziki nchini Kenya, Willy Paul, amewashangaza mashabiki wake baada ya kuandika ujumbe mzito wa majuto, akikiri kupoteza mwelekeo tangu alipoachana na muziki wa injili.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, msanii huyo ambaye kwa miaka kadhaa amekuwa akitamba upande wa muziki wa kidunia (secular), amefunguka kuwa moyo wake hauna amani na anahisi upweke wa kiroho.
Katika ujumbe wake, Willy Paul amedokeza kuwa huenda ni wakati wa kurejea kanisani, mahali ambapo alianzia safari yake ya sanaa, Amesema amegundua kuwa wito wake wa asili ni utumishi na uenezaji wa neno la Mungu kupitia kipaji chake.
Wakati baadhi ya mashabiki wakimpongeza kwa uamuzi huo wa ujasiri na kumkaribisha tena kwenye injili, wengine wamekuwa na shaka, wakijiuliza kama hii ni mbinu mpya ya kutaarifu ujio wa wimbo mpya (clout chasing).
Hata hivyo, uzito wa maneno yake safari hii unaonekana kugusa hisia za wengi, huku wadau wa muziki wa injili wakisubiri kuona kama kweli msanii huyo atarejea rasmi kwenye huduma ya injili.