Mkondo wa kwanza wa mechi nane za hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya unatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo na kesho, huku michezo ya marudiano ikipangwa kuchezwa Jumanne na Jumatano ijayo.
Katika ratiba ya leo, mabingwa wa Uturuki Galatasaray watawakaribisha vigogo wa Italia Juventus katika dimba la Rams Park, Uturuki. Wakati huo huo, Benfica watakuwa nyumbani katika Uwanja wa Da Luz kusaka ushindi dhidi ya mabingwa wa kihistoria wa Hispania Real Madrid.
Nchini Ujerumani, Borussia Dortmund watawakaribisha Atalanta katika Uwanja wa Signal Iduna Park, mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili. Nayo mechi ya mwisho ya leo itawakutanisha mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain dhidi ya wenzao AS Monaco katika dabi ya kusisimua ya Ligue 1 itakayohamishiwa kwenye anga la Ulaya.
Kesho, ratiba itaendelea ambapo Qarabag FK watakuwa uwanjani kusaka ushindi dhidi ya Newcastle United. Nchini Norway, Bodo/Glimt watamenyana na mabingwa wa Italia Inter Milan.
Katika mechi nyingine, Club Brugge watachuana na Atletico Madrid, huku Olympiacos wakifunga ratiba ya mkondo wa kwanza kwa kumenyana na Bayer Leverkusen.