Msanii nyota wa dancehall kutoka Jamaica, Vybz Kartel, amekanusha vikali taarifa zinazosambaa mitandaoni zikidai kuwa atafanya ziara ya muziki katika nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya, mwezi Mei 2026.
Kupitia taarifa rasmi, Kartel amesema kuwa yeye pamoja na timu yake ya usimamizi hawana ufahamu wowote kuhusu ziara hiyo inayodaiwa kupangwa katika eneo la Afrika Mashariki. Ameeleza wazi kuwa hakuna tamasha lolote lililotangazwa au kuthibitishwa na timu yake katika ukanda huo.
Msanii huyo ameonya mashabiki, waandaaji wa matamasha pamoja na kumbi za burudani kutoamini matangazo hayo. Amesema watu au majukwaa yanayodai kuwa yanahusika na maandalizi ya ziara hiyo yanafanya hivyo bila idhini yake na yanawapotosha wananchi.
Kartel pia amesisitiza kuwa mashabiki hawapaswi kutuma fedha kwa watu wanaojitambulisha kama waandaaji wa matamasha yake, kwani huenda ni utapeli unaolenga kuwadhulumu watu.
Aidha, msanii huyo ameeleza kuwa matangazo yote rasmi kuhusu maonyesho au ziara zake hutolewa kupitia kurasa zake zilizothibitishwa au kupitia wawakilishi wake waliothibitishwa pekee.