Mwanamuziki na mfanyibiashara maarufu wa Kenya, Akothee, ameandika ujumbe wa matumaini kwa mashabiki kupitia ukurasa wake wa Instagram akisimulia safari yake ya maisha iliyojaa changamoto na mafanikio yaliyotokana na bidii, nidhamu, na imani.
Katika ujumbe huo, Akothee amekiri kuwa hakuwahi kuaminiwa na watu wengi alipokuwa akikua. Amesema kwamba hata katika mambo madogo kama masomo na ndoa yake ya awali kijijini, watu hawakuona mustakabali mkubwa kwake.
Ameongeza kuwa licha ya wenzake kumzidi kwa hatua, aliendelea kuwashangilia kwa moyo mkunjufu na kusherehekea mafanikio yao bila wivu. Amesema kuwa sasa anajivunia kuona maisha yake yakiwa kwenye mstari, si kwa sababu kila kitu kiko sawa, bali amejifunza nidhamu na uthabitii unaomwezesha kukabiliana na changamoto za kila siku.
Mwanamama huyo amesisitiza kuwa uvumilivu umemjenga, neema imembeba, na imani yake kwa Mungu imekuwa nguzo kuu ya mafanikio yake. Hata hivyo amehitimisha ujumbe wake kwa kueleza kuwa Mungu wake ni Mungu wa kuishi, akiwatia moyo mashabiki wake kutokata tamaa licha ya magumu wanayopitia.