Msanii wa muziki wa Bongofleva wenye ladha ya R&B na Afro-pop, Christian Bella, amepewa rasmi uraia wa Tanzania baada ya kuishi nchini humo kwa muda mrefu na kutoa mchango mkubwa katika sekta ya sanaa.
Serikali imeeleza kuwa Christian Bella ameishi Tanzania kwa muda mrefu, ameanzisha familia, ana watoto na amejiunga kikamilifu na jamii ya Watanzania. Aidha, imesema kuwa amekuwa akiishi kwa kufuata sheria, kufanya kazi kwa uadilifu na kulipa malipo yote yanayotakiwa kisheria tangu alipoanza kuishi nchini humo.
Christian Bella alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini ameishi Tanzania kwa miaka mingi akijishughulisha na kazi za kisanii. Kupitia muziki wake, amejizolea umaarufu mkubwa na kuwa miongoni mwa wasanii waliotoa mchango muhimu katika kuikuza tasnia ya muziki wa Bongofleva ndani na nje ya nchi.
Hatua ya kumpa uraia msanii huyo imechukuliwa kama ishara ya kutambua mchango wa wahamiaji wanaoishi Tanzania kwa kufuata sheria na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.