Msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Dudu Baya, amezua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kutoa kauli nzito dhidi ya meneja wa wasanii Tanzania, Mkubwa Fella, akisema hata akipata taarifa za kifo chake hatahudhuria mazishi yake.
Akizungumza na Bongo24, Dudu Baya amemtaja Mkubwa Fella kama mtu mkatili aliyewanyanyasa wasanii wengi na kuzima vipaji vingi ndani ya tasnia ya muziki wa Bongo Fleva. Kwa mujibu wa msanii huyo, mateso na ukandamizaji unaodaiwa kufanywa na meneja huyo uliwaathiri wasanii wengi kiasi cha kuwaacha na maumivu makali.
Aidha, Dudu Baya amemkosoa mke wa Mkubwa Fella, akisema hana ufahamu wa kina kuhusu yaliyokuwa yakijiri nyuma ya pazia la tasnia hiyo, na kumtaka aache kuwashutumu wasanii kwa madai ya kukataa kumsaidia meneja huyo katika gharama za matibabu.
Kauli za Dudu Baya zimekuja siku chache baada ya taarifa za kuugua kwa Mkubwa Fella, ambapo mke wake alilalamika hadharani kuwa baadhi ya wasanii aliowahi kuwasaidia wamekataa kuchangia matibabu yake.