Msanii wa muziki wa Urbantone, Gody Tennor, amejitokeza kufafanua madai yaliyosambaa kuwa aliiba chain, iPad na laptop alipokuwa kwenye ziara yake nchini Australia.
Akizungumza katika mawasiliano ya simu na mtangazaji Tonny Mwirigi, msanii huyo amesema madai hayo si ya kweli, akieleza kuwa mali hizo alizipokea kama zawadi kutoka kwa shabiki wa kike aliyekutana naye wakati wa ziara hiyo.
Gody Tennor amesema kuwa hali ilibadilika baada ya blogu moja ya Kenya kuchapisha picha yake akiwa na mpenzi wake wakisherehekea kumbukumbu ya siku yao ya kuanzisha uhusiano, jambo lililomfanya shabiki huyo kuingiwa na wivu na baadaye kumtaka arudishiwe zawadi hizo.
Ameongeza kuwa alirudisha mali hizo siku moja baada ya kurejea nchini Kenya, akisisitiza kuwa hakuwahi kuiba wala kukiuka sheria.
Msanii huyo amewataka mashabiki na wadau wa sanaa kuepuka kuamini taarifa zisizothibitishwa zinazoweza kuharibu taswira ya wasanii.