Msanii nguli wa muziki wa reggae kutoka Jamaica, Luciano, amejiunga na mamilioni ya watu duniani wanaoomboleza kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Amolo Odinga.
Kupitia ujumbe wake Instagram, Luciano ameeleza masikitiko yake kwa kumpoteza Raila aliyekuwa na nafasi kubwa katika historia ya Kenya na bara la Afrika. Ametoa pole zake kwa familia ya Odinga na wananchi wote wa Kenya, akiwataka wabaki imara na kuendelea kuwa na imani katika kipindi hiki kigumu.
Luciano, anayefahamika kwa nyimbo zenye ujumbe wa amani na matumaini kama It’s Me Again Jah na Sweep Over My Soul, ameahidi kuzuru Kenya hivi karibuni kwa onyesho maalum la faraja, ili kuwatia moyo Wakenya kupitia muziki wake.
Hata hivyo msanii huyo amehitimisha salamu zake kwa kuimba wimbo wa kumuomboleza Raila Odinga, akimtaja kama kiongozi shujaa, mwenye maono na aliyejitoa kwa ajili ya watu wake.
Taarifa yake imepokelewa kwa hisia miongoni mwa mashabiki wa reggae na wafuasi wa Raila Odinga, wengi wakimsifu Luciano kwa kuonyesha upendo na mshikamano na wananchi wa Kenya katika kipindi hiki cha majonzi.