Mwigizaji wa filamu kutoka Kenya, Makena Kahuha, ametoa onyo kali kwa mabinti wanaotamani kujiunga na tasnia ya filamu, akiwataka wajihadhari dhidi ya rushwa ya ngono ambayo bado inatajwa kuwa changamoto kubwa katika sekta hiyo.
Kupitia mahojiano yake ya hivi karibuni, Makena amesema kuwa baadhi ya mabinti hujikuta wakilazimika kushiriki mapenzi na wanaume wenye ushawashi ili kupata nafasi za kazi, hali ambayo kwa muda mrefu huwarudisha nyuma badala ya kuwasaidia. Ameeleza kuwa pale mtu anapoanza kukubali masharti hayo, inakuwa vigumu sana kuvunja mzunguko huo.
Kwa mujibu wa Makena, mabinti wanapaswa kujisimamia na kuthamini vipaji vyao badala ya kukubali kudhalilishwa kwa kisingizio cha fursa. Amesisitiza kuwa tasnia ya filamu inahitaji mabadiliko ya kifikra, hasa kwa wale waliopewa dhamana ya kutoa nafasi za ajira.
Makena amewahimiza wasichana chipukizi kuzungumza wazi wanapokumbana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, huku akitoa wito kwa wadau wa tasnia hiyo kuweka mifumo salama na ya haki kwa kila msanii.