Naibu Rais wa Kenya, Kithure Kindiki, ameahidi kutoa msaada wa shilingi milioni tano kuwasaidia watoto wa marehemu mwimbaji wa injili Betty Bayo, aliyezikwa leo katika eneo la Mugumo Estate, Kaunti ya Kiambu.
Akihutubia waomboleza katika ibada ya mazishi, Kindiki amesema kuwa mara tu akaunti ya watoto hao itakapofunguliwa rasmi, atawasilisha msaada huo bila kuchelewa ili kuhakikisha wanaendelea na maisha bila changamoto.
Aidha, Kindiki amethibitisha kuwa Rais William Ruto pia ameahidi kutoa shilingi milioni tano kwa ajili ya kugharamia masuala ya elimu ya watoto wa marehemu, kama njia ya kumuenzi Betty Bayo na kutia nguvu mustakabali wa familia aliyoiacha nyuma.
Hotuba ya Naibu Rais ilipokelewa kwa shukrani na faraja kutoka kwa waombolezaji, waliomsifu marehemu Betty kama mwanamke aliyejitolea, mwenye kipaji na mchango mkubwa katika tasnia ya muziki wa injili.
Mazishi ya Betty Bayo yaliwaleta pamoja viongozi, wasanii na wananchi walioguswa na maisha yake, huku wasanii wa injili wakimsifu kama sauti ambayo itaendelea kuishi kupitia muziki na imani aliyoacha.