Mwili wa Karen Lojore, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Daystar mwenye umri wa miaka 20 aliyefariki dunia kufuatia mkanyagano uliotokea wakati wa tamasha la msanii wa Afrobeats Asake katika Uwanja wa kitaifa wa Nyayo, umezikwa rasmi leo nyumbani kwao Laikipia.
Hafla ya mazishi ilifanyika katika mazingira ya huzuni mzito huku ikihudhuriwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wanafunzi wenzake wa Daystar pamoja na wapendwa wengine waliokusanyika kumpa buriani ya mwisho na kusherehekea maisha yake.
Katika hotuba zao, wanafamilia wametaja Karen kama msichana mwenye ndoto kubwa, mnyenyekevu na aliyekuwa na mustakabali mzuri kielimu. Wanafunzi wenzake pia wamemtaja kama rafiki mwema, mchangamfu na mwenye moyo wa kusaidia wengine.
Kifo cha Karen kimeendelea kuzua majonzi makubwa na mjadala mpana kuhusu usalama katika matamasha makubwa nchini Kenya, huku mashabiki na wadau wa burudani wakitoa wito wa kuimarishwa kwa mipango ya usalama ili kuzuia matukio kama hayo kutokea tena.