Harmonize Atangaza Kukamilika kwa Albamu Mpya “31”
Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize, ametangaza rasmi kukamilika kwa albamu yake mpya inayojulikana kwa jina la “31”, akieleza kuwa kazi hiyo ni muhtasari wa maisha yake binafsi na safari ya muziki aliyopitia kwa miaka mingi. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize ameutaarifu umma kuhusu hatua hiyo muhimu katika taaluma yake, akifichua kuwa albamu hiyo imejaa hisia, uzoefu, mafunzo na mafanikio aliyopitia tangu alipoanza muziki. Katika albamu hiyo, msanii huyo ambaye pia ni mwanzilishi wa lebo ya Konde Music Worldwide, amewashirikisha wasanii wa kimataifa akiwemo nyota wa Nigeria Yemi Alade pamoja na msanii anayechipukia kwa kasi Draco. Mashabiki wake wamepokea taarifa hiyo kwa shangwe, wengi wakieleza kusubiri kwa hamu kusikia ladha mpya ya muziki kutoka kwa Harmonize ambaye amekuwa mstari wa mbele kusukuma muziki wa Afrika Mashariki katika majukwaa ya kimataifa. Ingawa tarehe rasmi ya kuachia albamu hiyo bado haijatangazwa, Harmonize ameahidi kuwa itakuwa kazi ya kipekee yenye ujumbe mzito na burudani ya hali ya juu kwa mashabiki wake kote duniani.
Read More