Harmonize Amvisha Rasmi Kajala Pete ya Uchumba Kwenye Yatch Party ya Kifahari

Harmonize Amvisha Rasmi Kajala Pete ya Uchumba Kwenye Yatch Party ya Kifahari

Msanii wa Bongo Fleva Harmonize amemvisha rasmi mwanamama Kajala Masanja pete ya uchumba katika hafla ya faragha iliyofanyika leo ndani ya boti, hatua iliyoashiria kurejea kwao rasmi katika mahusiano. Hafla hiyo maalum iliandaliwa kusherehekea mapenzi yao, ikihudhuriwa na marafiki wa karibu pekee. Wawili hao wameonekana wenye furaha na ukaribu mkubwa, hali iliyovutia mashabiki wao waliopata taswira za tukio hilo kupitia mitandao ya kijamii. Mpambe wa burudani Mwijaku, aliyekuwepo kwenye tukio la uchumba, amesema Harmonize amemheshimisha kwa kuhalalisha mahusiano yake na Kajala mbele ya zaidi ya watu 100 waliokuwapo, huku akiwatakia wawili hao baraka katika safari yao ya mapenzi. Hatua hii imekuja siku chache baada ya Harmonize kuthibitisha mahusiano yao juzi kati huko Zanzibar, ambako walizua gumzo kubwa baada ya kuonekana wakibadilishana mabusu hadharani mbele ya mashabiki.

Read More
 Harmonize na Kajala Washindwa Kujizuia Jukwaani, Wapigana Mabusu Hadharani

Harmonize na Kajala Washindwa Kujizuia Jukwaani, Wapigana Mabusu Hadharani

Msanii wa Bongo Fleva Harmonize na Mwanamama Kajala Masanja wamezua gumzo kubwa baada ya kuonekana wakishindwa kujizuia jukwaani na kupigana mabusu hadharani, tukio lililotokea usiku wa kuamkia leo wakati wa burudani huko Visiwani Zanzibar. Wakiwa mbele ya maelfu ya mashabiki, wawili hao walionekana wakitabasamu, kukumbatiana na hatimaye kubadilishana mabusu, jambo lililosababisha shangwe na makelele kutoka kwa mashabiki waliokuwepo. Kitendo hicho cha kupigana mabusu jukwaani kimezua tafsiri tofauti, huku baadhi ya mashabiki wakiamini ni ishara ya kurudiana rasmi, na wengine wakidai huenda ilikuwa ni sehemu ya burudani. Video na picha za tukio hilo zimesambaa kwa kasi mitandaoni, zikifanya jina la Harmonize na Kajala kutrendi. Bila shaka, tukio hili limeongeza ukurasa mpya katika simulizi la mahusiano ya Harmonize na Kajala, simulizi linaloendelea kuvuta hisia za wengi ndani na nje ya tasnia ya burudani.

Read More
 Harmonize Atangaza Kuachia Kolabo Tatu Disemba 25, Ikiwemo Ngoma na Mbosso

Harmonize Atangaza Kuachia Kolabo Tatu Disemba 25, Ikiwemo Ngoma na Mbosso

Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize, ametangaza rasmi kuwa ataachia ngoma tatu za kolabo tarehe Disemba 25 mwaka 2025, zikiwemo kazi zinazowahusisha wasanii wakubwa ndani na nje ya Afrika Mashariki. Kupitia Instagram stories, Harmonize amefichua kuwa miongoni mwa kolabo hizo ni ushirikiano wake wa kwanza kabisa na Mbosso. Katika maelezo yao kupitia mitandao ya kijamii, Harmonize na Mbosso wamezungumzia kwa pamoja mradi wao ujao, kila mmoja akimuelezea mwenzake kwa namna anavyomfahamu. Harmonize amemtaja Mbosso kama msanii mwenye kipaji cha kipekee na sauti yenye hisia, huku Mbosso akimpongeza Harmonize kwa ubunifu, uthubutu na mchango wake mkubwa katika kupeleka muziki wa Bongo Fleva kimataifa. Katika hatua nyingine, Harmonize pia ametangaza kuachia Kolabo na Focalistic, staa mkubwa kutoka Afrika Kusini pamoja naKolabo ya Yana Toma, ambayo pia inatajwa kuwa na ladha mpya na tofauti. Kwa sasa, macho na masikio ya wadau wa muziki yameelekezwa Disemba 25, siku ambayo Harmonize anatarajiwa kuwapa mashabiki wake zawadi ya Sikukuu kupitia kolabo hizi tatu zinazosubiriwa kwa hamu kubwa.

Read More
 Harmonize Aonesha Maendeleo ya Ujenzi wa Mjengo wake wa Kifahari

Harmonize Aonesha Maendeleo ya Ujenzi wa Mjengo wake wa Kifahari

Msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize, ameibua gumzo mitandaoni baada ya kuonyesha maendeleo ya ujenzi wa nyumba yake ya kifahari ya ghorofa. Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, bosi huyo wa lebo ya Konde Gang amepost video fupi (clip) akionekana akikagua mjengo wake mpya unaoendelea kujengwa. Katika clip hiyo, Harmonize anaonekana akitembea ndani na nje ya jengo hilo huku akitazama hatua mbalimbali za ujenzi. Licha ya kutoweka maelezo yoyote kwenye posti hiyo, Harmonize ametumia wimbo wake “I Made It” kama muziki wa background, jambo ambalo mashabiki wengi wametafsiri kuwa ni ishara ya kujivunia mafanikio yake binafsi pamoja na hatua ya mwisho ya kukamilika kwa mjengo huo. Hatua hiyo imewakumbusha wengi kauli ya Harmonize aliyotoa miaka kadhaa iliyopita alipodokeza kuwa alikuwa mbioni kujenga nyumba ya ghorofa. Wakati huo, baadhi ya watu walichukulia kauli hiyo kama mzaha, lakini sasa msanii huyo ameonekana kuthibitisha kuwa ndoto yake ilikuwa ya kweli.

Read More
 Harmonize Kuachia Albamu Mpya Januari 2026

Harmonize Kuachia Albamu Mpya Januari 2026

Msanii nyota wa Bongofleva, Harmonize, ametangaza rasmi kuwa ataachia albamu yake mpya mwezi Januari 2026, licha ya awali kuiahirisha kutokana na hali ya mashabiki kuwakataa baadhi ya wasanii waliojihusisha na siasa zilizosababisha machafuko nchini Tanzania. Kupitia taarifa yake, Harmonize amesema sasa kila kitu kipo tayari na amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kula ili kuipokea albamu hiyo mpya aliyoipa jina “31”, akiahidi itakuwa kazi kubwa yenye ubora wa hali ya juu na ladha tofauti ya muziki. Sanjari na hilo, msanii huyo pia ametangaza kufanya ziara kubwa ya kimataifa kuanzia Machi 15, itakayomkutanisha na mashabiki wake katika mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Sudan Kusini, Rwanda pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Kauli ya Harmonize imekuja baada ya kutangaza kuwa anatarajia kuwapa mashabiki wake zawadi ya nyimbo sita maalum kabla ya sikukuu za Krismasi za mwaka huu, hatua ambayo imeongeza hamasa na matarajio makubwa kuelekea albamu hiyo mpya.

Read More
 Harmonize: Sitaki Kuhusishwa Tena na Muziki wa Kiswahili

Harmonize: Sitaki Kuhusishwa Tena na Muziki wa Kiswahili

Staa wa muziki wa Bongofleva, Harmonize, ameweka wazi msimamo wake mpya wa kisanii kwa kusisitiza kuwa hataki kabisa kuhusishwa na muziki wa Kiswahili wala kulinganishwa na wasanii wanaoimba kwa lugha hiyo. Harmonize amesema yupo katika hatua muhimu ya mabadiliko ya kimkakati kwenye muziki wake, ambapo analenga kikamilifu soko la kimataifa kupitia kazi zinazotumia lugha ya Kiingereza. Kwa mujibu wake, safari yake ya sasa haiendani tena na muktadha wa muziki wa Kiswahili, jambo linalomfanya akatae kuwekwa kwenye mizani moja na wasanii wa miondoko hiyo. Msanii huyo ameongeza kuwa kuanzia sasa, hatarajii kutoa nyimbo nyingi kama ilivyozoeleka, akifichua kuwa mwaka 2026 hatakuwa na uzalishaji mkubwa wa kazi, bali ataweka nguvu kwenye ubora, viwango vya juu na utofauti wa kazi zake, badala ya kuendelea kufanya muziki wa Kiswahili au aina ileile kila wakati. Aidha, Harmonize amewajulisha mashabiki wake kuwa, licha ya msimamo huo mkali, atatoa nyimbo sita tarehe 25 Desemba kama zawadi maalum, huku akisisitiza kuwa nyimbo hizo ni sehemu ya mabadiliko yake mapya na si kurejea kwenye muziki wa Kiswahili. Katika ujumbe wake wa mwisho, Harmonize amesisitiza kuwa jina lake liheshimiwe kulingana na mwelekeo aliouchagua, akiwataka mashabiki na wadau wa burudani waache kabisa kumhusisha na muziki au wasanii wanaoimba Kiswahili, kwani anajiona tayari yupo kwenye ngazi nyingine ya kisanii na kimataifa.

Read More
 Harmonize Atangaza Vita na Mbunge Baba Levo kwa Kumhusisha na Diamond

Harmonize Atangaza Vita na Mbunge Baba Levo kwa Kumhusisha na Diamond

Msanii wa Bongo Fleva, Harmonize, ameibua taharuki mitandaoni baada ya kutangaza wazi kuwa yuko tayari kuzichapa na Baba Levo kufuatia kauli zinazomkera kutoka kwa mbunge huyo ambaye pia ni msanii na mtangazaji. Hii inakuja baada ya Baba Levo kudai kuwa Diamond Platnumz ndiye aliyemtoa Harmonize mavumbini, kauli ambayo Harmonize ameipinga vikali na kuiita ya kumdhalilisha. Ameeleza kuwa safari yake ya muziki imejengwa kwa damu, jasho, na juhudi binafsi si msaada wa mtu yeyote. Harmonize amesema amechoshwa na maneno ya Baba Levo na sasa yuko tayari kumkabili ana kwa ana ikiwa ndio lugha pekee atakayoielewa. Ameongeza kuwa ukimya wake umechukuliwa vibaya, na hivyo anataka kuweka mipaka na kulinda heshima yake. Harmonize ametoa msimamo mkali akiwataka wanaoandika habari kumhusu kuanza kwa kumtaja Mungu pekee, na si kumhusisha na mtu yeyote katika kutengeneza mafanikio yake. Kwa mujibu wa msanii huyo, kumhusisha na Diamond ni kutaka kumpotosha hadharani kuhusu safari ambayo ameijenga mwenyewe tangu akiwa chini kabisa kwenye muziki.

Read More
 Harmonize Adai Diamond Aliwavuruga Wasanii wa Label Yake Kwa Ahadi za Uongo

Harmonize Adai Diamond Aliwavuruga Wasanii wa Label Yake Kwa Ahadi za Uongo

Msanii wa Bongofleva Harmonize ameibua tuhuma nzito dhidi ya Diamond Platnumz, akidai kuwa yeye ndiye chanzo kikuu cha kuvunjika kwa lebo yake ya Konde Gang. Amedai kuwa Diamond alijihusisha moja kwa moja katika kuwavuruga wasanii aliokuwa amewalea, kwa kuwapa ahadi za uongo na kuwashawishi kuondoka kwenye lebo hiyo. Kulingana na Harmonize, Diamond aliahidi kumfadhili msanii Anjella katika matibabu yake pamoja na kumsaidia kupata kolabo na msanii Zuchu, jambo ambalo lilidaiwa kutumika kama chambo la kumtoa katika mwelekeo wa Konde Gang. Harmonize ameeleza kuwa ahadi hizo hazikuwahi kutimia na zimekuwa sehemu ya mikakati ya kuvuruga uongozi wake ndani ya lebo. Aidha, Harmonize amedai kuwa Diamond alimlipia Ibraah gharama za mawakili wakati msanii huyo alipotaka kujitoa Konde Gang, hatua ambayo anadai ilibuniwa ili kumvuta Ibraah ajiunge na kambi ya Wasafi au kuipunguzia nguvu lebo yake. Kwa mujibu wa maelezo yake, hatua hizo zote zimechangia kwa kiasi kikubwa kuyumba kwa lebo ya Konde Gang na kusababisha wasanii wake kukosa uthabiti na mwelekeo.

Read More
 Harmonize Akataa Kabisa Kuhusishwa na Diamond Platnumz

Harmonize Akataa Kabisa Kuhusishwa na Diamond Platnumz

Msanii wa Bongo Fleva, Harmonize, ameibua mjadala mkali mitandaoni baada ya kutoa onyo kali kwa watu wanaoendelea kumhusisha na Diamond Platnumz au kudai kwamba mafanikio yake yanatokana na msaada wa msanii huyo. Harmonize ameeleza kuwa kitendo cha baadhi ya watu kumweka chini ya Diamond ni kumvunjia heshima, akisisitiza kuwa yeye ni staa mkubwa kuliko Diamond na kwamba safari yake ya muziki imejengwa na juhudi zake mwenyewe. Amesema kuwa tayari amezungumza na mawakili wake, na mtu yeyote atakayemtaja katika muktadha wa kudai alisaidiwa na Diamond au kumhusisha na msanii huyo kwa namna yoyote, atamchukulia hatua kali za kisheria. Katika maelezo yake, Harmonize ameongeza kuwa Diamond hastahili heshima anayopewa kuhusu mafanikio yake kwa sababu ndiye aliyempeleka BASATA na kumtaka alipe milioni 600 bila huruma, na jambo hilo alilitekeleza. Amedai pia kuwa Diamond amekuwa akifurahia changamoto na anguko lake, hali inayomfanya asitake tena jina lake lihusishwe na msanii huyo.

Read More
 Harmonize Aahirisha Uzinduzi wa Album yake Mpya

Harmonize Aahirisha Uzinduzi wa Album yake Mpya

Msanii nyota wa Bongo Fleva, Harmonize, amelazimika kusitisha kwa muda uzinduzi wa albamu yake mpya “31” kutokana na hofu ya kususiwa na mashabiki kufuatia msimamo wake wa kisiasa katika uchaguzi wa Oktoba 29 nchini Tanzania. Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Harmonize amesema kuwa hatarajii albamu hiyo kutolewa mwaka huu kama ilivyopangwa awali, akibainisha kuwa mazingira ya sasa ya kisiasa yamechangia kuibua wasiwasi juu ya mapokezi ya kazi yake. Mkali huyo wa Best Couple, ameeleza kuwa ameanza mashauriano na uongozi wake ili kutathmini uwezekano wa kusogeza mbele tarehe rasmi ya kuachia albamu hiyo hadi mwaka 2026, wakati ambapo anatarajia joto la kisiasa litakuwa limetulia na mashabiki kurejea katika hali ya kawaida. Harmonize, ambaye amekuwa akifanya maandalizi ya albamu hiyo kwa miezi kadhaa, amesema anataka kazi zake zisikike katika mazingira huru bila mgawanyiko wa kisiasa kuathiri taswira yake kama msanii.

Read More
 Harmonize Ampongeza Davido kwa Kuwakumbuka Watanzania Waliofariki kwenye Machafuko ya Uchaguzi

Harmonize Ampongeza Davido kwa Kuwakumbuka Watanzania Waliofariki kwenye Machafuko ya Uchaguzi

Staa wa muziki wa Bongofleva Harmonize ameonekana kuguswa na kitendo cha msanii wa Nigeria Davido kusimamisha tamasha lake nchini Marekani ili kutoa heshima kwa Watanzania waliofariki wakati wa machafuko ya uchaguzi ya Oktoba 29. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize amepongeza hatua hiyo, akitoa wito wa maombi ya pamoja kwa nchi za Tanzania, Sudan Kusini, Nigeria na Afrika kwa ujumla, ili amani itawale na waliopoteza maisha wapumzike kwa amani. Harmonize ametoa kauli hiyo alipokuwa akitoa maendeleo ya Albamu yake mpya 31 ambayo kwa mujibu wake huenda ikakosa kutoka mwaka huu kutokana na sababu ambazo hakuziweka wazi. Mkali huyo wa ngoma ya Best Friend, amesema kwa sasa ameanzisha mchakato wa mazungumzo na uongozi wake kuhusu mipango ya kuachia kazi hiyo mwaka 2026.

Read More
 Harmonize Afunguka Sababu za Kunyoa Kipara

Harmonize Afunguka Sababu za Kunyoa Kipara

Staa wa Bongo Fleva Harmonize amejibu lawama na dhana zilizokuwa zikisambaa mtandaoni baada ya mashabiki na wadau mbalimbali kudai kuwa amemuiga msanii wa Nigeria, Asake, kutokana na muonekano wake mpya wa kunyoa kipara. Kupitia InstaStory, ameweka wazi kuwa uamuzi wake wa kunyoa kipara hauna uhusiano wowote na msanii huyo wa Afrobeat kama inavyodaiwa. Amesema kuwa aliamua kubadili muonekano wake kwa sababu maalum inayomhusu mwanasiasa mashuhuri wa Kenya, Hayati Raila Odinga. Mkali huyo wa ngoma ya Best Couple, ameeleza kuwa kunyoa kipara ilikuwa ni ishara ya kumuenzi na heshima kwa kiongozi huyo ambaye alimuita Baba. Ameongeza kuwa hakutaka kutangaza jambo hilo mapema, lakini baada ya kuona mashabiki wameupenda muonekano huo, ataendelea kuubaki nao. Kwa siku kadhaa, mashabiki wamekuwa wakifananisha sura mpya ya Harmonize na ile ya Asake, wakimtuhumu msanii huyo wa Konde Gang kwa kuiga mtindo wa kunyoa kipara.

Read More