Mshindi mara mbili wa msururu wa gofu wa DP World, Haydn Porteous kutoka Afrika Kusini, atawaongoza wachezaji wengine 120 waliothibitisha kushiriki mkondo wa tano wa Sunshine Tour, utakaofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 mwezi ujao jijini Kigali, Rwanda.
Porteous, ambaye pia aliwahi kutwaa taji la Kenya Open, ni miongoni mwa wachezaji kutoka mataifa 16 watakaoshiriki katika mashindano hayo. Mataifa hayo ni pamoja na Kenya, Rwanda, Uganda, Tanzania, Nigeria, Zimbabwe, Ghana, Cameroon, Malawi, Zambia, Côte d’Ivoire, Burundi, Afrika Kusini, Misri, Canada na Uingereza.
Rwanda, ikiwa mwenyeji wa mashindano haya, itawakilishwa na wachezaji 29, akiwemo Celestin Nsanzuwera, aliyeshinda mkondo wa Sunshine Tour uliofanyika mapema mwaka huu huko Diani, Kaunti ya Kwale.
Kenya itawakilishwa na wachezaji waandamizi akiwemo Njoroge Kibugu, Dismas Indiza, Daniel Nduva, Rizwan Charania, Greg Snow, Mutahi Kibugu na Simon Ngige. Kwa upande wa wanawake, Kenya itawakilishwa na Naomi Wafula, Irene Nakalembe na Lillian Koowe, ambao wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa mchezo wa gofu nchini na kanda ya Afrika Mashariki.