Entertainment

Wasanii na wanahabari waomboleza kifo cha Raila Odinga

Wasanii na wanahabari waomboleza kifo cha Raila Odinga

Sekta ya burudani na vyombo vya habari nchini Kenya zimeingia katika majonzi makubwa kufuatia taarifa za kifo cha kiongozi wa upinzani na mwanasiasa mkongwe, Raila Amolo Odinga, ambaye amefariki dunia nchini India kutokana na mshtuko wa moyo.

Kifo chake kimezua simanzi kote nchini humo, huku wadau wa sekta ya burudani na habari wakijitokeza kutoa rambirambi zao kupitia mitandao ya kijamii.

Wasanii na wanahabari wameelezea Raila kama kiongozi wa kipekee aliyekuwa na uhusiano wa karibu na vijana, wakiwemo wabunifu na waandishi wa habari. Wengi wamesema Raila alikuwa na uelewa mpana wa umuhimu wa sanaa na vyombo vya habari katika kukuza taifa, na mara nyingi alionekana kuhudhuria hafla za burudani, mikutano ya kijamii na matamasha ya vijana.

Baadhi ya watangazaji na wanahabari wamesema Raila alikuwa nguzo muhimu katika kuhimiza uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari, akiamini kwamba taifa lenye demokrasia thabiti lazima liruhusu sauti tofauti kusikika. Wameeleza kuwa kifo chake kimeacha pengo lisilo na mfano katika historia ya kisiasa na kijamii nchini Kenya.

Mitandao ya kijamii imefurika jumbe za huzuni na kumbukumbu za maisha ya Raila, huku maelfu ya wananchi, wasanii, waandishi wa habari na viongozi wakitumia alama za reli kama #RIPRailaOdinga, #RestInPeaceBaba, na #ThankYouBaba kueleza hisia zao. Wengine wamechapisha picha na video za matukio ya zamani zikionyesha Raila akishirikiana na vijana na kushiriki matukio ya kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *