Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Zuchu, ameonyesha furaha na upendo wake baada ya kukutana ana kwa ana na pacha wake kutoka Kenya anayemwigiza.
Binti huyo, ambaye mashabiki wanamuita “Zuchu wa Mchongo”, amejizolea umaarufu mitandaoni kutokana na kumwigiza Zuchu katika mitindo ya uchezaji na mavazi, sambamba na kufanya challenges za nyimbo zake. Kutokana na kufanana kwao kimuonekano, mara nyingi mashabiki huchanganyikiwa kumtambua nani ni nani.
Katika video iliyosambaa, Zuchu alionekana akimkumbatia dada huyo kwa upendo na kumshukuru kwa namna anavyounga mkono kazi zake za muziki. Msanii huyo wa WCB alikiri wazi kwamba anamthamini na anafarijika kuona kazi zake zikileta nafasi ya kuibua vipaji vipya hata nje ya Tanzania.
Mashabiki mitandaoni wamefurahishwa na ukaribu huo, wakibainisha kuwa ni jambo la kipekee kwa Zuchu kumtambua na kumpongeza mtu anayemwigiza badala ya kuona kama ni ushindani.