Mwanamuziki nyota wa Afrobeat, Burna Boy, ameomba radhi kwa mashabiki wake kufuatia wimbi la lawama lililotanda mtandaoni, baada ya madai kuibuka kwamba aliwaita baadhi ya wafuasi wake masikini.
Kupitia ujumbe mrefu alioutoa mtandaoni, Burna Boy amejitetea akisema kuwa mara nyingi matendo yake mema hayapewi nafasi, lakini akifanya jambo lolote linaloonekana kama kosa, ndipo linapoenezwa kwa kasi kubwa.
Mkali huyo wa Afrobeat, amefafanua kuwa maneno yake yalipotoka yalikuwa ni sehemu ya utani aliokuwa akifanya na bendi yake kuhusu jambo tofauti kabisa, lakini yakapotoshwa na kuwasilishwa kana kwamba alidharau mashabiki wake.
Hata hivyo ametoa msimamo wake kwamba anawapenda wanaompenda na kuwaheshimu wanaomheshimu. Licha ya kusisitiza kuwa hakukosea katika tukio hilo, Burna Boy amewaomba radhi kwa yeyote aliyekasirishwa au kuhisi kuathirika na tafsiri hiyo, akisema kuwa yeye pia ni binadamu na si mkamilifu.