Staa wa Bongo Fleva Harmonize amejibu lawama na dhana zilizokuwa zikisambaa mtandaoni baada ya mashabiki na wadau mbalimbali kudai kuwa amemuiga msanii wa Nigeria, Asake, kutokana na muonekano wake mpya wa kunyoa kipara.
Kupitia InstaStory, ameweka wazi kuwa uamuzi wake wa kunyoa kipara hauna uhusiano wowote na msanii huyo wa Afrobeat kama inavyodaiwa. Amesema kuwa aliamua kubadili muonekano wake kwa sababu maalum inayomhusu mwanasiasa mashuhuri wa Kenya, Hayati Raila Odinga.
Mkali huyo wa ngoma ya Best Couple, ameeleza kuwa kunyoa kipara ilikuwa ni ishara ya kumuenzi na heshima kwa kiongozi huyo ambaye alimuita Baba. Ameongeza kuwa hakutaka kutangaza jambo hilo mapema, lakini baada ya kuona mashabiki wameupenda muonekano huo, ataendelea kuubaki nao.
Kwa siku kadhaa, mashabiki wamekuwa wakifananisha sura mpya ya Harmonize na ile ya Asake, wakimtuhumu msanii huyo wa Konde Gang kwa kuiga mtindo wa kunyoa kipara.