Lebo ya muziki ya Chief Loot Music inayomilikiwa na Bilionea Chief Godlove, imetoa taarifa rasmi ili kuondoa sintofahamu kwa wasanii wanaotamani kusainiwa na lebo hiyo.
Kupitia taarifa hiyo, uongozi wa lebo hiyo umesisitiza kuwa muziki ni biashara na si msaada, hivyo wasanii wanapaswa kuelewa na kukubaliana na masharti ya mkataba kabla ya kusaini.
Kwa mujibu wa lebo hiyo, mkataba wao unadumu kwa kipindi cha miaka kumi. Baada ya kusaini, msanii atapatiwa makazi pamoja na usafiri wa gari, huku lebo ikisimamia mahitaji muhimu kama studio, utayarishaji wa video za muziki, promosheni, mavazi, chakula na fedha za matumizi binafsi.
Katika mgawanyo wa mapato, lebo hiyo itachukua asilimia 80 ya mapato, huku msanii akipata asilimia 20 kwa kipindi chote cha mkataba.
Aidha, lebo hiyo imeeleza kuwa masuala binafsi ya msanii kama matatizo ya kifamilia, ndoa au mahusiano hayahusiani na shughuli za lebo.
Wakati huo huo, Chief Loot Music imetangaza kuwa itamtambulisha rasmi msanii wake wa kwanza Machi 9, 2026, siku ambayo pia inaadhimisha siku ya kuzaliwa ya mkurugenzi wa lebo hiyo.