Mtangazaji maarufu nchini Tanzania, Mwijaku, ametuma ujumbe mzito kwa vijana na watumiaji wa mitandao ya kijamii akiwataka kumuenzi marehemu MC Polepole kwa kumuombea dua badala ya kupakia picha zake mtandaoni.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Mwijaku amesema kuwa imekuwa kawaida kwa watu wengi kushindana kupost picha za marehemu kwenye mitandao, huku wakisahau kuwa namna bora zaidi ya kuwaenzi wapendwa ni kwa maombi na matendo mema.
Mwijaku ambaye anafahamika kama DC wa Instagram, ameeleza kuwa kama kulikuwa na haja ya kushirikiana au kumwonyesha upendo MC Polepole mitandaoni, hiyo ilipaswa kufanyika wakati akiwa hai, na si baada ya kifo chake.
Hata hivyo amehimiza vijana kutumia muda huu kumuombea marehemu ili Mungu aipokee roho yake na amweke mahali pema peponi, akibainisha kuwa hilo ndilo jambo la maana na lenye heshima zaidi kwa marehemu kuliko kusambaza picha zake mitandaoni.