Mwenyekiti wa Washereheshaji Mkoa wa Dodoma Meshack Sudai amekanusha vikali taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa watu waliodai kuwa ndugu wa marehemu MC Pilipili, wakisema kuwa mwili wa mchekeshaji huyo umepatikana na majeraha mabaya.
Akizungumza jana, Sudai amesema taarifa hizo si za kweli na kwamba familia ya marehemu haijatoa tamko lolote rasmi hadi sasa. Ameeleza kuwa kinachoendelea kusambazwa mtandaoni ni uvumi unaopaswa kupuuzwa mpaka pale taarifa kamili kutoka kwa familia zitakapowekwa wazi.
Mwenyekiti huyo maarufu kwa jina la MC Mwakitwange, amefafanua kuwa kikao cha familia kinatarajiwa kuketi ili kujadili mwenendo wa uchunguzi unaoendelea na ndipo tamko rasmi litakapowasilishwa kwa umma na wadau wa tasnia ya burudani.
Sudai amesisitiza jamii kuwa na subira na kuheshimu familia ya marehemu katika wakati huu mgumu, akiwataka wananchi na wafuasi wa MC Pilipili kusubiri taarifa sahihi kutoka kwa familia na mamlaka husika.
MC Pilipili alifariki ghafla Jumapili, Novemba 16 2025 huko Dodoma ambako inadaiwa alisafiri kwa ajili ya kusherehesha moja ya hafla ya harusi.