Msanii nyota wa muziki wa Uganda, Eddy Kenzo, hatimaye amenyosha maelezo kuhusu mvutano kati yake na mwanamuziki Bebe Cool kuhusiana na fedha zilizodaiwa kutolewa kwa wasanii wakati wa kampeni za Rais Yoweri Museveni.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Kenzo ameeleza kuwa hajawahi kuzuia bodi ya chama cha NRM kumpa fedha Bebe Cool, bali alishauri tu chama hicho kuhusisha wasanii wa maeneo mbalimbali nchini Uganda katika mipango ya kampeni.
Hitmaker huyo wa Nsimbudde, amesema alipoalikwa katika ofisi ya Katibu Mkuu wa chama, alitoa pendekezo kwamba kila mkutano wa kampeni ujumuishwe na wasanii watano wa wilaya mbalimbali pamoja na wale wanaotoka Kampala, na wazo hilo lilikubaliwa.
Kwa mujibu wa Kenzo, lengo lake lilikuwa kuhakikisha wasanii wote nchini humo wananufaika na fursa hizo, na si kuingilia majukumu ya Bebe Cool ambaye bado ndiye anayeongoza miradi hiyo.
Kenzo pia amesisitiza kuwa hana tatizo lolote na Bebe Cool, akibainisha kwamba wanaendelea kushirikiana kwa ajili ya manufaa ya chama cha NRM na Rais Museveni.
Kwa takribani wiki moja sasa, kumekuwepo na madai kwamba Kenzo alizuia uongozi wa NRM kutoa fedha kwa Bebe Cool na badala yake alipendekeza mpango mbadala kupitia Uganda National Musicians Federation (UNMF), unaohusisha kushirikisha wasanii wa mikoani ili kupunguza gharama za kampeni.
Ripoti zinasema pendekezo hilo halikupokelewa vyema na baadhi ya wasanii akiwemo Bebe Cool, Gravity Omutujju, Jose Chameleone, na Catherine Kusasira, jambo lililozua mvutano kati ya kambi hizo mbili.