Msanii nyota wa Bongo Fleva, Harmonize, amelazimika kusitisha kwa muda uzinduzi wa albamu yake mpya “31” kutokana na hofu ya kususiwa na mashabiki kufuatia msimamo wake wa kisiasa katika uchaguzi wa Oktoba 29 nchini Tanzania.
Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Harmonize amesema kuwa hatarajii albamu hiyo kutolewa mwaka huu kama ilivyopangwa awali, akibainisha kuwa mazingira ya sasa ya kisiasa yamechangia kuibua wasiwasi juu ya mapokezi ya kazi yake.
Mkali huyo wa Best Couple, ameeleza kuwa ameanza mashauriano na uongozi wake ili kutathmini uwezekano wa kusogeza mbele tarehe rasmi ya kuachia albamu hiyo hadi mwaka 2026, wakati ambapo anatarajia joto la kisiasa litakuwa limetulia na mashabiki kurejea katika hali ya kawaida.
Harmonize, ambaye amekuwa akifanya maandalizi ya albamu hiyo kwa miezi kadhaa, amesema anataka kazi zake zisikike katika mazingira huru bila mgawanyiko wa kisiasa kuathiri taswira yake kama msanii.