Msanii wa muziki kutoka Uganda, Kin Bella, amezua gumzo kubwa baada ya kufichua changamoto nzito zinazokabili wasanii wa kike chipukizi wanaotaka kufanikiwa katika tasnia ya muziki nchini humo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mtangazaji Sheilah Price, Bella amesema kuwa wasanii wengi wa kike nchini humo hulazimika kukubali kutumika kimapenzi na watu wenye ushawishi mkubwa ili kupenya na kufanikiwa katika tasnia ya muziki.
Bella amesema kuwa changamoto za kifedha na ukosefu wa fursa huwafanya wasanii chipukizi, hasa wanawake, kuingia katika mahusiano yasiyo rasmi ili kupata msaada wa kurekodi nyimbo, kutengeneza video na kujitangaza. Ameongeza kuwa mara nyingi kipaji pekee hakitoshi bila kuwa na mtu mwenye nguvu au ushawishi nyuma ya msanii.
Msanii huyo ametoa wito kwa wadau wa tasnia ya muziki nchini Uganda kuweka mifumo ya haki na uwazi itakayowawezesha wasanii wa kike kufanikiwa kwa misingi ya vipaji vyao, bila kushinikizwa kukubali mahusiano ya kimapenzi.