Msanii wa muziki wa injili Solomon Mkubwa amefunguka kuhusu sababu nzito iliyopelekea kupoteza mkono wake wa kulia, akieleza kuwa tukio hilo lilitokana na kile anachodai kuwa mashambulizi ya giza alipokuwa bado mtoto.
Kwenye mahojiano yake hivi karibuni, Solomon amesema mkasa huo ulitokea alipokuwa na umri wa takribani miaka 12, kipindi ambacho familia yao ilikuwa inapitia mgogoro mkubwa baada ya baba yake kuoa mke wa pili. Kwa mujibu wa msanii huyo, mvutano kati ya mke wa kwanza na wa pili ulisababisha chuki zilizomfikia yeye kama mtoto, hali aliyodai ilimfanya kulengwa na uchawi uliouathiri mkono wake wa kulia.
Amesema mkono huo ulianza kuharibika vibaya kiasi kwamba madaktari hawakuwa na njia nyingine ila kuukata ili kuokoa maisha yake, baada ya hali kuwa mbaya sana. Solomon anaamini kilichompata hakikuwa cha kawaida, bali kilihusisha mashambulizi ya kiroho yaliyobadilisha kabisa maisha yake.
Licha ya maumivu na changamoto alizopitia, msanii huyo amesema amejifunza kusamehe na kuendelea na maisha. Ameongeza kuwa wimbo wake “Nimewasamehe Wote” aliutoa kama sehemu ya safari yake ya uponyaji, akisema uliimbwa kwa hisia nzito kutokana na yaliyompata na hasa kumpoteza mkono wake wa kulia.