WhatsApp imeanza majaribio ya mfumo mpya unaolenga kuongeza usalama wa watoto wanaotumia jukwaa hilo, kwa kuruhusu wazazi kufungua akaunti maalum kwa ajili ya watoto wao.
Kwa mujibu wa taarifa ya WhatsApp, mfumo huo utatumia mpangilio wa “Secondary Account” ambayo itakuwa ni akaunti ya mtoto. Akaunti hiyo itatumia namba tofauti ya simu lakini itaunganishwa moja kwa moja na akaunti ya mzazi au mlezi, itakayojulikana kama “Primary Account” (akaunti kuu).
Kupitia mfumo huu, mzazi au mlezi atakuwa na uwezo wa kudhibiti baadhi ya mipangilio muhimu ya akaunti ya mtoto, ikiwemo kuamua ni watu gani wataruhusiwa kuwasiliana naye. Hata hivyo, WhatsApp imesisitiza kuwa mzazi hataweza kusoma wala kuona mazungumzo (chats) ya mtoto wake, hatua inayolenga kulinda faragha ya mtumiaji mdogo.
WhatsApp imesema lengo la mfumo huu ni kuweka uwiano kati ya usalama wa watoto na haki yao ya faragha, huku wazazi wakipata zana za msingi za ulinzi bila kuingilia mawasiliano binafsi ya watoto wao.
Mfumo huu mpya unafanana na mipangilio ya udhibiti wa wazazi (parental controls) inayotumika kwenye majukwaa mengine ya kidijitali kama Instagram, TikTok, YouTube, pamoja na Apple Accounts, ambayo tayari yamekuwa yakitoa akaunti maalum kwa watoto zilizounganishwa na akaunti za wazazi.