Mwanamuziki mkongwe kutoka Uganda Jose Chameleone amelazwa hospitalini na kufanyiwa upasuaji wa jicho baada ya kupoteza uwezo wa kuona katika jicho lake la kulia.
Kupitia taarifa aliyoshiriki akiwa hospitalini, Chameleone, amesema kuwa alipoteza uwezo wa kuona katika jicho lake la kulia kwa kasi, hali iliyomlazimu kutafuta matibabu ya haraka na kufanyiwa upasuaji maalum ili kuzuia madhara makubwa zaidi.
Katika ujumbe wake wa shukrani, amemwomba Mungu amjalie uponyaji wa haraka huku akitoa pongezi kwa Dkt. Ludovica Tindebwa pamoja na timu nzima ya Hospitali ya Kampala Eye Lasik kwa kufanikisha upasuaji wake na kumpa huduma bora wakati wa matibabu.
Kwa sasa, hali yake inaelezwa kuwa imara baada ya upasuaji huo kufanyika kwa mafanikio, huku akiendelea na uangalizi wa kitabibu.