Rapa Toxic Lyrikali ameapa kutoyumba wala kupoteza mwelekeo wake wa kimuziki kutokana na kile alichokiita diss track bandia kutoka kwa baadhi ya marapa wa Kenya.
Akijibu moja kwa moja mashambulizi kutoka kwa kundi la Buruklyn Boyz, ambao awali walitoa diss track iliyozua gumzo mitandaoni iitwayo Stima, Toxic amesema kuwa hataruhusu bifu za mitandaoni kumvuruga katika safari yake ya kujijenga kisanii.
Katika baadhi ya mistari ya wimbo wake mpya uitwao Dumpsite, Toxic amedai kuwa wakati akijenga brand yake kwa juhudi na nidhamu, baadhi ya wanaomkosoa walikuwa wakifanya muziki wa kihuni mitaani bila mwelekeo maalum. Ameongeza kuwa mafanikio aliyoyafikia hayakuja kwa bahati, bali ni matokeo ya miaka ya kazi ngumu, ubunifu na uthabiti.
Rapa huyo ameenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa itachukua muda mrefu kwa marapa anaowaita bandia kufikia mafanikio yake, iwapo wataendelea kuendekeza wivu badala ya kufanya kazi kwa bidii. Kwa mujibu wake, muziki ni ushindani wa vipaji na si bifu za kijinga.
Hii ni mara ya kwanza kwa Toxic kujibu diss track kwa kuingia studio na kuachia ngoma rasmi, hatua inayodhihirisha jinsi alivyochukulia kwa uzito mashambulizi kutoka kwa Buruklyn Boyz.